Uchambuzi wa kitabu: The self-employed life by Jeffrey shaw.
KUHUSU MWANDISHI
Jeffrey Shaw ni mjasiriamali aliyejiajiri katika tasnia ya upigaji picha (Photography), mnenaji, kocha wa biashara na mshauri wa ukuzaji wa chapa (Brand). Pia anaendesha biashara ya podcast na ameandika vitabu vinavyohusu maisha na safari ya kujiajiri.
NENO LA UTANGULIZI KWA WEWE ULIYEJIAJIRI
Unapaswa kujishukuru na kujipongeza kwa uamuzi wa kujiajiri, kwa sababu kupitia shughuli zako unachangia katika uchumi wa Taifa, unaendesha familia yako na unatoa huduma au bidhaa zinazowasaidia watu wengine.
Hata hivyo, kujiajiri si mwisho wa safari. Ni mwanzo wa safari inayohitaji ukuaji binafsi, mikakati ya kibiashara na tabia nzuri za kila siku.
Mwandishi anaonesha kuwa mafanikio ya biashara yanategemea mambo matatu makuu:
Mosi: Ukuaji wako binafsi (Personal Development).
Pili: Mikakati ya kibiashara (Business Strategies).
Tatu: Tabia za mafanikio za kila siku (Daily Habits).
MWANZONI UKITAKA KUANZISHA BIASHARA AU ENEO LAKO LA KUJIAJIRI
1. ANZA NA MUUNDO WA FIKRA
Hatua ya kwanza ni kujijenga wewe mwenyewe. Jifahamu na tambua uwezo ulio nao.
Jiulize:
✓ Mimi ni nani?
✓ Nina nguvu gani?
✓ Ninataka nini katika maisha yangu?
✓ Ninaweza kufanya nini ili kupata ninachokitaka?
✓ Ni hatua gani ninapaswa kuanza kuchukua?
Kisha chukua hatua na kila unapopata mafanikio, jifunze kuyatunza na kuyaendeleza.
Mchakato huu unaweza kuangaliwa kupitia:
BE → DO → HAVE
Kwanza kuwa mtu unayetaka kuwa (Be), kisha fanya mambo yanayohitajika (Do), ndipo upate matokeo unayotaka (Have).
2. JIAJIRI KWA SABABU YENYE MAANA
Usijiajiri kwa sababu tu umechoshwa na ajira.
Jiulize kwa nini unataka kujiajiri.
Sababu zinaweza kuwa:
✓ Unataka kuacha alama.
✓ Unataka kuwa na uwezo mkubwa wa kuamua kuhusu maisha yako.
✓ Unataka kukua.
✓ Unataka kufanya mambo kwa namna tofauti.
Sababu yenye nguvu inaweza kukusaidia kuvumilia changamoto utakazokutana nazo katika safari hiyo.
3. ELEWA KUWA BIASHARA NI SAFARI YA KUJIFUNZA
Biashara ina mchakato wa kujaribu, kukosea, kujifunza na kuboresha.
Utafanya maamuzi ambayo baadaye utaona hayakuwa sahihi. Utakosea, utashindwa na wakati mwingine utajiuliza kama ulifanya uamuzi sahihi wa kuanza.
Muhimu si kutokosea kabisa.
Muhimu ni kujifunza kutokana na makosa na kuboresha maamuzi yanayofuata.
4. JIUNDIE MIFUMO BORA YA UENDESHAJI
Usiiendeshe biashara kwa kutegemea kumbukumbu, nguvu zako binafsi au juhudi za kila siku pekee.
Jenga mifumo inayokusaidia kupata matokeo kwa uthabiti.
Mifumo inaweza kuwa katika:
- Mauzo;
- Masoko;
- Huduma kwa wateja;
- Fedha;
- Uzalishaji;
- Usimamizi wa wafanyakazi;
- Ufuatiliaji wa matokeo.
5. CHAGUA WATEJA WANAOTAMBUA THAMANI YAKO
Si kazi yako kumshawishi kila mtu kwamba unastahili kuchaguliwa.
Tambua watu wanaohitaji kile unachotoa na wanaoweza kutambua thamani yake.
Fahamu mteja wako, tatizo lake na matokeo anayoyataka.
6. WAWEZESHE WATEJA WAKUCHAGUE
Fahamu soko lako na wape wateja sababu ya kukuchagua.
Usiuze bidhaa pekee; waoneshe namna bidhaa au huduma yako inaweza kuwasaidia kufikia matokeo wanayotaka.
Mteja hanunui tu kile unachouza; mara nyingi hununua thamani na matokeo anayotarajia kupata.
7. JIPIME KAMA UNA UWEZO WA KUFIKIA MATOKEO UNAYOYATAKA
Kila unapokwama kufikia kiwango fulani cha mafanikio, jiulize:
“Je, nina uwezo unaohitajika kuvutia na kutengeneza matokeo ninayotaka?”
Kama jibu ni ndiyo, endelea kuboresha michakato inayozalisha matokeo.
Kama jibu ni hapana, anza kwanza kujenga uwezo unaokosekana.
8. KAMA UMASKINI NI KERO, TAFUTA NJIA YA KUONDOKA KWENYEKE
Kama hali yako ya kifedha haikuridhishi, usiizoe hali hiyo kiasi cha kuiona kuwa ndiyo maisha yako ya kudumu.
Tumia kutoridhika huko kama msukumo wa kujifunza, kuongeza kipato, kujenga biashara na kuboresha maisha yako.
Usichukie hali yako kiasi cha kukata tamaa; ichukie kiasi cha kuchukua hatua.
9. VIKWAZO NI SEHEMU YA SAFARI
Kila jambo kubwa unaloliendea linaweza kuwa na vikwazo.
Wajibu wako si kuviepuka vyote, bali kujifunza namna ya kuvishughulikia na kuvishinda pale inapowezekana.
Watu wanaopiga hatua si wale wasiokutana na vikwazo, bali ni wale wanaojifunza kukabiliana navyo.
10. KAMA HUONI SABABU YA KUJIAJIRI, ANDIKA UNACHOTAKA KUACHANA NACHO
Kama bado hujui kwa nini unataka kujiajiri, jiulize ni mambo gani hutaki yaendelee kuwa sehemu ya maisha yako.
Kwa mfano:
i) Kutaka kuboresha hali yako ya kifedha.
ii) Kutaka kuwa na udhibiti zaidi wa muda na kazi yako.
iii) Kutaka kuondokana na hali ya kutothaminiwa au kutotambuliwa.
iv) Kutaka kujenga kitu chako mwenyewe.
Sababu hizi zinaweza kukusaidia kuelewa unachotafuta kupitia kujiajiri.
MASWALI MATATU YA KUJIULIZA ILI KUSHINDA VIKWAZO
11. JIULIZE MASWALI SAHIHI
Moja: Ni fikra gani hasi ninazotumia muda mwingi kuzifikiria na ninapaswa kuziacha?
Fikra hizo zinaweza kuwa:
- Hofu;
- Kujiona hutoshei;
- Kuahirisha mambo;
- Kutaka kuwa mkamilifu kabla ya kuanza;
- Kujiambia huwezi.
Mbili: Ni imani gani ninazopaswa kuziacha ili nipige hatua?
Kwa mfano:
- “Siwezi.”
- “Sijawahi kufanya jambo kubwa.”
- “Mimi si mtu wa mafanikio.”
Tatu: Ni fikra zipi bora ninazohitaji kujenga?
Kwa mfano:
- Kujifunza zaidi;
- Kuchukua hatua;
- Kupunguza muda wa kulalamika;
- Kutafuta suluhisho badala ya kukosoa tu;
- Kujenga uwezo unaohitajika.
FANYA MAMBO HAYA NA YATAKUSAIDIA KUPIGA HATUA
12. KUWA NA UWEZO WA KUJUA UNATAKA NINI
Usiseme tu:
“Nataka kufanikiwa.”
Eleza mafanikio unayoyataka.
Kwa mfano:
“Nataka kuongeza kipato changu kutoka Tsh X hadi Tsh Y ndani ya mwaka mmoja.”
Au:
“Nataka kuongeza mauzo yangu kutoka Tsh X hadi Tsh Y ndani ya miezi sita.”
Kisha:
ii) Weka nia thabiti ya kufikia lengo hilo.
iii) Jitoe vya kutosha kufanya kile kinachohitajika.
iv) Fanya jambo kila siku linalokusogeza kuelekea unachotaka.
v) Ukikutana na kushindwa, jifunze na ujaribu tena.
MIKAKATI YA KIBIASHARA — BUSINESS STRATEGY
13. MAFANIKIO TOFAUTI MARA NYINGI YANATOKA KWENYE MIFUMO TOFAUTI
Kama unaona wengine wanafanya vizuri zaidi katika biashara kuliko wewe, usiangalie matokeo pekee.
Jiulize:
Wanafanya nini tofauti?
Ili kukuza biashara:
Moja: Fanya masoko kuwa kipaumbele cha biashara yako.
Pili: Jifunze kuliona soko kama sehemu ya kujenga biashara, si jambo la kulichukia.
Tatu: Kutana na wateja mahali walipo na elewa mahitaji yao.
Nne: Wafurahie wateja wako.
Tano: Wafahamu wateja wako kwa kina kiasi cha kuwapa kile wanachohitaji.
Sita: Elewa kwamba watu hupendelea kufanya biashara na biashara inayowajali na kuwaheshimu.
Saba: Jiamini katika thamani unayowapa wateja wako na waeleze kwa uwazi.
Nane: Toka nje ya biashara yako mara kwa mara ili kuona mambo ambayo huenda huyatambui ukiwa ndani ya shughuli za kila siku.
Tisa: Tengeneza ofa yenye thamani na inayoeleweka kwa mteja.
Kumi: Badala ya kuiona marketing kama “kuwasukuma watu wanunue”, ione pia kama mchakato wa kuwavuta na kuwaingiza watu sahihi katika biashara yako (enrolling).
14. AINA SITA ZA WATU KATIKA SAFARI YA MTEJA
Mwandishi anaeleza hatua mbalimbali ambazo mtu anaweza kupitia kabla na baada ya kuwa mteja:
Mosi — Lurkers
Hawa wanakuona lakini bado hawajakufuata au kujihusisha moja kwa moja.
Pili — Curious
Hawa wameanza kuwa na hamu na wanaweza kukufuata ili wajifunze zaidi.
Tatu — Engaged
Hawa wameanza kujihusisha na maudhui yako, kwa mfano kulike, kucomment au kushiriki.
Nne — Connected
Hawa una mawasiliano nao na mnaanza kujenga uhusiano wa moja kwa moja.
Tano — Client
Hawa tayari wamenunua bidhaa au huduma yako.
Sita — Hug
Hawa ni watu ambao umejenga nao uhusiano wa karibu zaidi na wa muda mrefu.
Hivyo, safari ya mteja haianzi siku anayofanya malipo. Mara nyingi huanza mapema zaidi kupitia kuona, kufuatilia, kuhusika, kuwasiliana na kujenga uaminifu.
15. JENGA BIASHARA YENYE VYANZO VINGI VYA MAPATO
Mwandishi anajadili wazo la Business Model of Multiples—kujenga biashara yenye njia zaidi ya moja za kuzalisha mapato.
Kwa mfano, biashara inayojihusisha na kilimo inaweza kuwa na shughuli nyingine zinazohusiana na uwezo wake mkuu, kama:
- Ufugaji;
- Uvuvi;
- Ushauri;
- Mafunzo;
- Utafiti;
- Uchambuzi;
- Mentorship kwa taasisi na kampuni za kilimo;
- Teknolojia;
- Mazingira;
- Na huduma nyingine zinazohusiana na utaalamu wake.
Lengo si kufanya kila kitu bila mpangilio.
Lengo ni kujenga vyanzo mbalimbali vya mapato vinavyotokana na uwezo, rasilimali, wateja na soko ulilonalo.
Kwa hiyo, usipanue biashara kwa sababu tu umeona fursa nyingine. Jiulize kwanza:
“Je, fursa hii ina uhusiano na uwezo wangu mkuu, wateja wangu au mfumo wa biashara yangu?”
Hapo ndipo diversification inapoweza kuwa na maana zaidi kuliko kujitawanya.



